Mar 08, 2019 07:54 UTC
  • Shambulizi la kigaidi karibu na Ikulu ya Rais laua watu kadhaa Somalia

Kwa akali watu saba wameuawa huku wengine tisa wakijeruhiwa katika mripuko wa bomu na hujuma ya ufayatuaji risasi iliyofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mashuhuda wanasema shambulizi hilo la kigaidi lilifanyika jana Alkhamisi karibu na kituo kikuu cha upekuzi, katika lango la kuingia katika Ikulu ya Rais mjini Mogadishu ambapo saba waliuawa.

Wanasema sauti kubwa ya mripuko ilisikika katika eneo hilo na kufuatiwa na milio ya risasi. Wingu la moshi mweusi lilitanda katika eneo la tukio baada ya mripuko huo wa bomu.

Adan Ahmed, afisa wa polisi mjini Mogadishu amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, watu watano wakiwemo raia na askari ndio waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Hata hivyo kundi la wanamgambo wa al-Shabaab linadai kuwa limeua wanajeshi 10 wa Somalia katika hujuma hiyo. 

Magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi mara kwa mara ndani na nje ya Somalia

Hujuma hiyo imetokea siku chache baada ya Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia kukiri kuwa, vita dhidi ya kundi hilo la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab havitamalizika hivi karibuni, lakini akasisitiza kuwa genge hilo limedhoofishwa kwa kiasi kikubwa.

Alkhamisi ya wiki iliyopita, magaidi hao wakufurishaji walifanya shambulizi jingine dhidi ya Hoteli ya Makka al-Mukarram mjini Mogadishu, ambapo watu wasiopungua 30 waliuawa.

Tags