Wanawake 9 na viongozi wa upinzani wasukumwa jela Sudan
Naibu Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Umma na binti ya kinara wa chama hicho ni miongoni mwa wanawake tisa wa upinzani waliohukumiwa kifungo jela kwa tuhuma za kukiuka sheria ya hali ya hatari nchini Sudan.
Mahakama hiyo ya Khartoum imemhukumu kifungo cha wiki moja jela Naibu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Umma Mariam Sadiq al-Mahdi pamoja na wanawake wengine wa upinzani, mbali na kuwatoza faini ya pauni elfu 2 za Sudan (dola 42) kwa kushiriki maandamano 'haramu'.
Mariam Sadiq al-Mahdi ni binti wa mkuu wa chama cha Umma, Sadiq al Mahdi ambaye alikuwa waziri mkuu wa mwisho aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini Sudan.
Sadiq al-Mahdi aliondolewa madarakani mwaka 1989 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Rais wa sasa wa Sudan, Omar al Bashir.
Siku kadhaa zilizopita Rais wa Sudan alivunja serikali na kutangaza hali ya hatari nchi nzima na kisha akawafuta kazi magavana wa mikoa yote ya nchi hiyo na nyadhifa hizo kukabidhiwa wanajeshi.

Sudan inashuhudia maandamano ya wananchi tangu Disemba 19 mwaka jana wanaolalamikia hali ngumu ya kiuchumi na kupanda bei za bidhaa muhimu khususan bei ya mkate na petroli.
Viongozi wa serikali ya Sudan wametangaza kuwa hadi sasa waandamanaji 30 wameuawa, katika hali ambayo asasi za kiraia zimetangaza kuwa zaidi ya watu 50 wameuliwa katika ghasia na machafuko huko Sudan.