Rais wa Afrika Kusini asema haiwezekani kuzuia tena mageuzi ya ardhi
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema wazungu wanaomiliki vipande vikubwa vya ardhi hawawezi tena kuendelea akupinga sera za marekebisho ya ardhi ambazo serikali yake imeazimia kutekeleza.
Amesema kufanyika polepole kwa mageuzi ya ardhi nchini Afrika Kusini kumefanya umma ukose uvumilivu, na sasa kuna haja ya kuyaharakisha ili kurekebisha makosa ya kihistoria.
Rais Ramaphosa amesema hayo wakati akikabidhi hati za ardhi kwa watu wenye asili ya Griqua na Khpis mjini Cape Town, ambao ni watu waliochanganya damu na kukumbwa na historia ndefu ya kunyang'anywa ardhi. Rais Ramaphosa amesema kukabidhiwa ardhi hiyo kwa wamiliki wa awali ni tukio la kihistoria, kwa sababu ni takwa la kwanza la wakaazi wa jimbo la Cape Magharibi.
Rais Ramaphosa pia amesema serikali ina lengo la pamoja la kuboresha maisha ya Waafrika Kusini wote na hali yao kimali, kwa kuwapa ardhi. Hata hivyo amesema mageuzi ya ardhi hayatayumbisha sekta ya kilimo, kuhatarisha usalama wa chakula, au kuhatarisha ongezeko la uchumi na kuongeza nafasi za ajira.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini aliyechukua nafasi ya Jacob Zuma mwezi Februari mwaka jana, amelipa kipaumbele kikubwa suala la kugawa ardhi kwa wazalendo weusi katika jitihada zake za kukiunganisha tena chama tawala cha ANC na kupata uungaji mkono wa umma kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo mwakani.
Umiliki wa ardhi na mashamba ni suala nyeti sana nchini Afrika Kusini ambako ubaguzi wa rangi ungali umekita mizizi baada ya miongoni miwili ya kuondolewa madarakani utawala wa ugauzi (apartheid) uliowapokonya Wazalendo weusi mashamba yao na kuyagawa kwa wazungu waliowachache. Hivi sasa Waafrika Kusini asili wanataka kurejeshewa ardhi zao za jadi zilizonyakuliwa na makaburu wakati wa zama za utawala wa ubaguzi wa rangi.