Afrika Kusini yaitisha mkutano na mabalozi wa Afrika baada wageni kushambuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52536-afrika_kusini_yaitisha_mkutano_na_mabalozi_wa_afrika_baada_wageni_kushambuliwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Lindiwe Sisulu anatarajiwa kuitisha mkutano wa dharura na mabalozi wa Afrika kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni mjini Durban na Polokwane.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 31, 2019 10:13 UTC
  • Afrika Kusini yaitisha mkutano na mabalozi wa Afrika baada wageni kushambuliwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Lindiwe Sisulu anatarajiwa kuitisha mkutano wa dharura na mabalozi wa Afrika kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni mjini Durban na Polokwane.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  na Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa, waziri ana wasiwasi juu ya wimbi la mashambulizi yanayoelekezwa dhidi ya raia wa kigeni na mali zao. Sisulu ameyataka mashirika ya utekelezaji wa sheria kuwazuia wahusika ambao wanawalenga wahajiri kutoka nchi za Afrika.

 Ameongeza kuwa kampuni za Afrika Kusini na wananchi wake wanakaribishwa na kupendwa katika bara hilo, hivyo amewataka wananchi kurejesha ukarimu kwa ukarimu.Lindiwe Sisulu 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Lindiwe Sisulu

Amewasisitiza wananchi wa Afrika Kusini kutosahau jukumu lililobebwa na mataifa mengine ya Afrika kusaidia nchi hiyo ili kupigania ukombozi wakati wa utawala wa makabaru na hatimaye kupata uhuru na demokrasia.

Kwa upande wake rais Cyril Ramaphosa amesema amekasirishwa na vitendo hivyo vya kuwahujumu raia wa kigeni na kusema 'havikubaliki.

Ramaphosa amesema vitendo hivyo vinaonyesha kutostahamiliana na ni utovu wa shukurani kwa nchi za Afrika ambazo zilihusika mojw akwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kusaidia Afrika Kusini katika mapambano yake ya muda mrefu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Jumapili na Jumatatu iliyopita magenge yalihujumu maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni mjini Durban na kupora mali. Mwanamke mmoja anaripotiwa kupoteza maisha yake wakati akijiaribu kukimbua wakati wa vurumai hizo huku watu wengine wawili na wakipigwa risasi. Rais wa kigeni walikimbilia hifadhi katika msikiti na kituo cha polisi baada ya hali kuwa mbaya zaidi.