UNHCR: Watu 6 wameuawa katika hujuma dhidi ya wahajiri Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52558-unhcr_watu_6_wameuawa_katika_hujuma_dhidi_ya_wahajiri_afrika_kusini
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeeleza wasiwasi wake kutokana na wimbi la kushambuliwa raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2019 10:39 UTC
  • UNHCR: Watu 6 wameuawa katika hujuma dhidi ya wahajiri Afrika Kusini

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeeleza wasiwasi wake kutokana na wimbi la kushambuliwa raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema, mashambulizi hayo yanayowalenga raia wa kigeni wakiwemo wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi katika miji ya Durban na Polokwane katika mkoa wa Kwazulu-Natal, yamesababisha vifo vya watu sita na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Makundi ya watu waliobeba marungu, visu na mapanga yalivamia nyumba za raia wa kigeni na kuwafukuza, huku wakipora mali zao. Kadhalika maduka kadhaa yanayomilikiwa na raia hao wa wageni yalivamiwa huku kiasi kikubwa cha bidhaa zikiibiwa, kuharibiwa au kuchomwa moto.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Lindiwe Sisulu anatarajiwa kuitisha mkutano wa dharura na mabalozi wa Afrika kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni mjini Durban na Polokwane.

Maafisa wa polisi Afrika Kusini wakijaribu kutuliza hali

Kwa upande wake Rais Cyril Ramaphosa amesema amekasirishwa na vitendo hivyo vya kuwahujumu raia wa kigeni na kusema 'havikubaliki.

Ramaphosa amesema vitendo hivyo vinaonyesha kutostahamiliana na ni utovu wa shukurani kwa nchi za Afrika ambazo zilihusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kusaidia Afrika Kusini katika mapambano yake ya muda mrefu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.