Waalgeria washadidisha maandamano baada ya kuteuliwa rais wa mpito
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52735-waalgeria_washadidisha_maandamano_baada_ya_kuteuliwa_rais_wa_mpito
Maelfu ya wananchi wa Algeria wakiwemo wanafunzi wa Vyuo Vikuu wamemiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kuteuliwa rais wa mpito wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 09, 2019 14:41 UTC
  • Waalgeria washadidisha maandamano baada ya kuteuliwa rais wa mpito

Maelfu ya wananchi wa Algeria wakiwemo wanafunzi wa Vyuo Vikuu wamemiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga kuteuliwa rais wa mpito wa nchi hiyo.

Mkuu wa Baraza la Seneti la nchi hiyo, Abdelkader Bensalah ndiye aliyeteuliwa hii leo kuchukua nafasi hiyo ya kuongoza nchi kwa muda wa siku 90 kabla ya kufanyika uchaguzi mpya.

Hata hivyo baada ya kuapishwa kuchukua nafasi hiyo, maelfu ya wananchi wamejitokeza katika maandamano dhidi ya uteuzi wake, wakisema kuwa Bensaleh pamoja na Waziri Mkuu Nouredine Bedoui na Tayeb Belaiz, Mkuu wa Baraza la Katiba aliyepokea barua ya kujiuzulu Boutefika ni watu waliokuwa karibu na rais huyo aliyejiuzulu, hivyo wote wanapaswa kuondoka ofisini.

Baada ya kuapishwa, Bensalah ambaye ameteuliwa kuwa rais wa muda kwa mujibu wa katiba, ameliambia Bunge kuwa, "Tunapaswa kuwaruhusu Waalgeria wamchague rais wao haraka iwezekanavyo."

Abdelkader Bensalah, Rais wa Mpito wa Algeria

Jumanne iliyopita, Abdelaziz Bouteflika aliyeiongoza Algeria kwa muda wa miaka 20 alikabidhi barua yake ya kujiuzulu urais kwa Baraza la Katiba la nchi hiyo na hivyo kuhitimisha uongozi wake wa miongo miwili katika nchi hiyo.

Mnamo mwezi Februari mwaka huu, Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni anayugua ugonjwa kiharusi alitangaza kuwa atagombea tena urais kwa muhula wa tano mfululizo, tangazo ambalo liliibua wimbi la malalamiko makubwa na upinzani mkali wa wananchi na kumfanya kiongozi huyo abadilishe uamuzi wake na kujizulu.