AMISOM yaomba msamaha kwa kuua raia wa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5281-amisom_yaomba_msamaha_kwa_kuua_raia_wa_somalia
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimetoa taarifa rasmi ya kuomba msamaha kwa kuua 'kimakosa' raia wanne wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2016 23:33 UTC
  • AMISOM yaomba msamaha kwa kuua raia wa Somalia

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimetoa taarifa rasmi ya kuomba msamaha kwa kuua 'kimakosa' raia wanne wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa hiyo imesema kuwa, askari wa AMISOM Jumamosi iliyopita walilifyatulia risasi gari lililokataa kusimama katika kituo cha upekuzi katika mji wa Buulo Mareer jimbo la Shebelle ya Chini na kuua raia wanne waliokuwemo kwenye gari hilo wakidhani ni wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab, lenye mfungamano na mtandao wa kimataifa wa al-Qaeda.

AMISOM imesema gari hilo lilipokataa kusimama katika kituo cha upekuzi iliamini kuwa ni la al-Shabaab na lina mada za miripuko.

Kikosi cha Kusimamia Amani cha AU kimetuma salamu za rambi rambi kwa familia za watu wanne waliouawa na kusema kuwa kinasikitika kuua raia wasio na hatia katika tukio hilo lililofanyika jimbo la Shebelle ya Chini, yapata kilomita 80 kusini mwa mji mkuu Mogadishu. Kamisheni ya Umoja wa Afrika imeanzisha uchunguzi kubaini kiini na mazingira ya kuuawa raia hao wa Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye uhusiano na mtandao wa al-Qaida limekuwa likitekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya maafisa wa serikali ya Somalia na vikosi vya kulinda amani vya kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili sasa.