HRW yataka kukamatwa walioshambuliwa wahamiaji nchini Afrika Kusini
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito wa kufunguliwa mashitaka watu waliohusika na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.
Ripoti ya HRW ilieleza kwamba katika muda wa siku tatu Machi 25 hadi Machi 27 makundi ya watu waliokuwa na vyuma na marungu walivunja nyumba za raia wakigeni na kuwafurusha mjini Durban, Mashariki mwa Pwani ya Afrika kusini na kisha kupora mali zao.
Mkurugenzi wa HRW nchini Afrika Kusini, Dewa Mavhiga amesema, ili kukomesha vitendo vya kushambuliwa raia wakigeni, kuna udharura wa kuwa na kanuni bora, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka wahusika haraka iwezekanavyo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, mashambulizi hayo yaliyowalenga raia wa kigeni wakiwemo wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi katika miji ya Durban na Polokwane katika mkoa wa Kwazulu-Natal, yalisababisha vifo vya watu sita na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Makundi ya watu waliobeba marungu, visu na mapanga yalivamia nyumba za raia wa kigeni na kuwafukuza, huku wakipora mali zao. Kadhalika maduka kadhaa yanayomilikiwa na raia hao wa wageni yalivamiwa huku kiasi kikubwa cha bidhaa zikiibiwa, kuharibiwa au kuchomwa moto.
Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo alikemea vikali mashambulizi hayo, na kusisitiza kuwa vitendo hivyo vya kuwahujumu raia wa kigeni 'havikubaliki" na kwamba vinaonyesha kutostahamiliana na ni utovu wa shukurani kwa nchi za Afrika ambazo zilihusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kusaidia Afrika Kusini katika mapambano yake ya muda mrefu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.
Hadi sasa raia wa kigeni wasiopungua 62 wameuliwa tangu kuanza kwa wimbi la mashambulizi dhidi ya wageni hao mwaka 2008.