Iran na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wao wa kiulinzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53307-iran_na_afrika_kusini_kuimarisha_ushirikiano_wao_wa_kiulinzi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimetoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano wa muda mrefu wa kiulinzi na kijeshi baina yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2019 06:35 UTC
  • Iran na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wao wa kiulinzi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimetoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano wa muda mrefu wa kiulinzi na kijeshi baina yao.

Mwito huo ulitolewa jana Jumapili hapa mjini Tehran, katika kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na kiulinzi wa nchi mbili hizi, wakiongozwa na Jenerali Mohammad Ahadi, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran na Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Afrika Kusini.

Jenerali Ahadi amesema nchi mbili hizi zitaendelea kushirikiana na kubadilishana mawazo sanjari na kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi wa pande mbili, kwa lengo la kufikia mikakati ya pamoja ya muda mrefu ya kiulinzi na kijeshi.

Huku akishiria kuhusu hatua za kiuhasama na zilizo kinyume cha sheria za Marekani, Jenerali Ahadi amesema kitendo cha hivi karibuni cha Washington cha kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH (IRGC) katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, kwa mara nyingine imeweka bayana uadui mkubwa wa nchi hiyo ya kibeberu kwa taifa hili.

Ramani zenye bendera za Iran na Afrika Kusini

Kadhalika amebainisha kuwa wananchi wa Iran wataendelea kumheshimu na kumuenzi hayati Mzee Nelson Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini, kwa jitihada zake za kupambana kwa amani na ubaguzi wa rangi uliokuwa umekita mizizi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Oktoba mwaka jana, Jenerali Ahadi ambaye pia ni mkuu wa masuala ya kimataifa wa Wizara ya Ulinzi ya Iran, akiwa mjini Pretoria, Afrika Kusini kuhudhuria kikao cha pili cha tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini, alisema, sifa maalumu za kijiopolitiki na irada ya kisiasa waliyonayo viongozi wa Iran na Afrika Kusini, zinaandaa mazingira mwafaka ya kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili hususan katika uga wa ulinzi.

Disemba 13 mwaka 2016, nchi mbili hizi zilitia saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi.