UN yatoa mwito wa kusitishwa mapigano kwa muda nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53308-un_yatoa_mwito_wa_kusitishwa_mapigano_kwa_muda_nchini_libya
Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL kimezitaka pande husika kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja kuanzia leo Jumatatu, katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2019 06:40 UTC
  • UN yatoa mwito wa kusitishwa mapigano kwa muda nchini Libya

Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL kimezitaka pande husika kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja kuanzia leo Jumatatu, katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Katika taarifa, UNSMIL imevitaka vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa kundi linalojiiita Jeshi la Kitaifa la Libya na vile vya Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya visitishe kwa muda mapigano hayo yanayoendelea kushuhudiwa katika mji mkuu Tripoli, wakati huu ambapo mwezi mtukufu wa Ramadhani unaanza.

Kadhalika ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umezitaka pande hasimu kuruhusu ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu kwa wale wanaoihitaji, sambamba na kuhakikisha kuwa raia wa mji mkuu huo wanaruhusiwa kutembea kwa uhuru katika kipindi hicho cha usitishaji vita.

Hii ni katika hali ambayo, Jenerali Khaftar amevitaka vikosi vyake vishadidishe mapigano katika mwezi huu mtufuku wa Ramadhani, akidai kuwa eti mwezi huu ni mwezi wa jihadi.

Khalifa Haftar alipokutana na Mfalme wa Saudia mjini Riyadh Machi 27

Jenerali huyo muasi alianza kuushambulia mji wa Tripoli muda mfupi baada ya kufanya safari huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia; ambapo iliarifiwa kuwa alipewa mamilioni ya dola na watawala wa Aal-Saud kwa ajili ya kuanzisha vita hivyo.

Watu karibu 400 wameuawa hadi sasa tangu kuanza kushambuliwa mji mkuu Tripoli na wengine 1650 wamejeruhiwa, mbali na zaidi ya 50 elfu kulazimika kuyahama makazi yao.