Al Shabab 14 watiwa mbaroni nchini Somalia
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Somalia imesema kuwa, nchi hiyo imeshadidisha operesheni zake za kiusalama na kijasusi dhidi ya kundi la al Shabab, operesheni ambazo zimefanikisha kutiwa mbaroni wanamgambo 14 wa kundi hilo.
Shirika la habari la Xinhua limeripoti habari hiyo leo na kumnukuu Muallim Shukri, msemaji wa Wizara ya Usalama wa Taifa ya Somalia akisema mjini Mogadishu kwamba, operesheni hizo zimefanyika katika maeneo ya Wadajir na Hodan mjini Mogadishu na kufanikiwa kuwatia mbaroni magaidi 14 wa al Shabab.
Shukri amewataka wananchi wa Somalia wazidi kushirikiana na serikali katika kutoa taarifa kuhusiana na mahali wanapojificha magaidi wa al Shabab.
Kwa mujibu wa habari hiyo, mwezi uliopita pia, polisi wa Somalia waliua wanamgambo wasiopungua 70 wa al Shabab katika jimbo la Puntland na kuwatia mbaroni zaidi ya 30 wengine.
Huko nyuma kundi la al Shabab lilikuwa linadhibiti maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Somalia lakini mwaka 2015 lilipoteza miji mikubwa liliyokuwa linaidhibiti na kubakiwa na baadhi ya maeneo hasa ya vijijini.