Chama cha ANC chasherehekea ushindi Afrika Kusini
Maelefu ya wafuasi wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC Jumapili walimiminika katika mitaa ya mji wa Johannesburg na maeneo mengine wakisherehekea ushindi wa bunge uliofanyika wiki hii ambapo chama hicho kimetangazwa kuwa mshindi licha ya umashuhuri wake kupungua.
Chama cha ANC kilipata ushindi wa asilimia 57.5 ya viti bungeni kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi siku ya Jumamosi.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na chama cha Democratic Alliance huku chama cha EFF kinachoongozwa na Julius Malema, mwanachama wa zamani wa ANC, kikichukua nafasi ya tatu.
Rais Cyril Ramaphosa amejiunga na wafuasi wa chama hicho, kusherehekea ushindi huo katika makao makuu ya chama hicho.
Chama hicho cha zamani cha ukombozi cha Nelson Mandela hakijawahi kupata chini ya asilimia 60 ya kura katika uchaguzi wa taifa tangu kilipoingia madarakani nchini Afrika Kusini kupitia uchaguzi wa kwanza uliowahusisha watu wote mwaka 1994.
Uchaguzi huu ndio changamoto ya kwanza kubwa tangu Cyril Ramaphosa alipochukua nafasi ya rais wa nchi kutoka kwa Jacob Zuma, aliyekumbwa na kashfa kadhaa mnamo Februari 2018.
Katika uchaguzi uliopita mwaka 2014, chama cha ANC kilishinda asilimia 62 ya kura, chama cha DA kilipata asilimia 22 na EFF asilimia 6.