Chama tawala chashinda uchaguzi wa Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53445-chama_tawala_chashinda_uchaguzi_wa_afrika_kusini
Baada ya kura za uchaguzi wa Bunge la Afrika Kusini kumalizika kuhesabiwa, chama tawala cha African National Congress ANC, kwa mara nyingine kimefanikiwa kupata wingi wa vita katika bunge hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2019 00:29 UTC
  • Chama tawala chashinda uchaguzi wa Afrika Kusini

Baada ya kura za uchaguzi wa Bunge la Afrika Kusini kumalizika kuhesabiwa, chama tawala cha African National Congress ANC, kwa mara nyingine kimefanikiwa kupata wingi wa vita katika bunge hilo.

Hivyo chama hicho kilichopata asilimia 58 ya kura zilizopigwa kimepata fursa nyingine ya kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika uchaguzi huo nafasi ya pili imechukuliwa na chama cha Democratic Alliance kilichopata asilimia 20.70 huku chama cha EFF kinachoongozwa na Julius Malema, mwanachama wa zamani wa ANC, kikichukua nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 10.63 ya kura.

Huu umekuwa uchaguzi wa sita kuandaliwa nchini Afrika Kusini tokea kumalizika kwa kipindi cha ubaguzi wa rangi nchini humo mwaka 1994. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, chama kinachopata wingi wa vita bungeni ndicho hupewa fursa ya kumchagua rais wa nchi. Utendaji wa chama tawala cha ANC katika miaka michache iliyopita umekuwa ukikidhoofisha taratibu na kukifanya kipoteze imani ya waungaji mkono wake chini. Hata kama chama hicho kimeweza kushinda uchaguzi wa hivi karibuni lakini kimepoteza umashuhuri wake na kukabiliwa na changamoto nyingi. Ufisadi, kudorora uchumi, kuongezeka kiwango cha ukosefu wa ajira na mgogoro wa nishati ni baadhi ya changamoto muhimu zinazoikabili Afrika Kusini kwa sasa. Vyama vya upinzani vinasema kuwa changamoto hizo zinatokana na utendaji dhaifu wa chama tawala na hivyo kukipelekea kupoteza umashuhuri wake wa huko nyuma.

Nembo ya chama tawala Afrika Kusini ANC

Akijadili suala hilo, Mmusi Maimane, kiongozi wa chama cha Democratic Alliance anasema: Wasiwasi na masikitiko makubwa ni kwamba viongozi waliochaguliwa na wananchi badala ya kuingoza jamii, hivi sasa wanaiba na kupora mali ya watu masikini.

Hali ya sasa Afrika Kusini, kuongezeka kwa malalamiko ya wananchi na kushindwa serikali kutatua matatizo yao na hasa ya kiuchumi na kijamii ni jambo ambalo limepelekea kuimarika kwa shughuli za vyama vya upinzani nchini humo na hasa vinavyoonekana kuwa na misimamo ya kupindukia mipaka. Chama vya Democratic Alliance DA na cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi, Economic Freedom Fighters EFF, ambavyo vimekuwa vikipiga nara za kupinga ubeberu na watu weupe, hivi sasa vimepata umashuhuri na ushawishi mkubwa Afrika Kusini. Vyama hivyo vinafanya juhudi kubwa za kuongeza ushawishi wao katika mfumo wa madaraka wa nchi hiyo kwa kukikosoa mara kwa mara chama tawala na kusema kuwa hakina tena uwezo wa kutatua matatizo ya Waafrika Kusini, na hasa ya kiuchumi na kijamii. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kuwa chama tawala kitapitia kipindi kigumu katika siku zijazo. Ni kwa msingi huo ndipo Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo akaahidi katika kampeni zake za uchaguzi kwamba atakifanyia chama cha ANC mabadiliko makubwa na ya kimsingi kwa lengo la kupambana na ufisadi nchini.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini (kulia) akiwa na Jacob Zuma aliyejiuzulu kutokana na kashfa nyingi zilizomkabili

Ramaphosa ambaye ni mmoja wa watu waliokuwa karibu sana na Nelson Mandela, shujaa wa mapambano dhidi ya mfumo wa kibaguzi wa Apartheid, aliingia madarakani baada ya kujiuzulu Jacob Zuma aliyekabiliwa na kashfa mbalimbali za kimaadili na ubadhirifu wa pesa za umma. Rais huyo ameahidi kupigania haki za Waafrika Kusini na kutatua matatizo yao ya msingi kwa lengo la kuinua kiwango chao cha maisha.

Ni wazi kuwa kupungua umashuhuri wa chama tawala katika uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo ni kengele ya tahadhari kwa viongozi wa sasa wa Afrika Kusini. Kwa kutilia maanani msukumo mpya wa vyama vya upinzani na malalamiko ya wananchi, inaonekana kuwa hivi karibuni Rais Cyril Ramaphosa atakuwa kwenye njia panda na wakati mdogo sana wa kuweza kutekeleza ahadi alizotoa.