Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini: Niko tayari kuachia ngazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53496-rais_salva_kiir_wa_sudan_kusini_niko_tayari_kuachia_ngazi
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema yuko tayari kuachia ngazi na kukabidhi madaraka iwapo kutakuwa na haja ya msingi ya yeye kuchukua hatua hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 15, 2019 01:55 UTC
  • Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini: Niko tayari kuachia ngazi

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema yuko tayari kuachia ngazi na kukabidhi madaraka iwapo kutakuwa na haja ya msingi ya yeye kuchukua hatua hiyo.

Rais Kiir aliyasema hayo jana mjini Juba na kufafanua kuwa, "Sio azma yangu kuendelea kusalia madarakani kwa kipindi kirefu. Watu wanaofanya niendelee kuwa uongozini ni wale wenye kukwamisha mchakato wa amani."

Amesema ukwamishaji huo unawanyima Wasudan Kusini fursa ya kushiriki uchaguzi na kuamua mustakabali wa nchi yao. Kiir ameongeza kuwa, ghasia na machafuko hayawezi kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo.

Baadaye jana Rais Kiir alilihutubia bunge la nchi hiyo, na kumuasa hasimu wake Riek Machar kumuunga mkono katika mchakato wa kurejesha amani ya kudumu katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Rais Kiir (kulia) na Riek Machar

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Rais Kiir kudai kuwa, uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa unapasa kuakhirishwa kwa muda wa mwaka mmoja licha ya makubaliano ya amani ya mwezi Septemba mwaka jana yaliyohitimisha vita vya ndani nchini humo kuanisha Mei 12 kuwa tarehe ya mwisho ya kuakhirishwa mchakato huo.

Aidha alipinga pendekezo la kiongozi wa zamani wa waasi Riek Machar aliyetaka kuundwa serikali hiyo katika kipindi cha miezi sita. Machar ambaye alitia saini mapatano hayo ametaka utekelezwaji wake uakhirishwe kwa muda wa miezi 6 ili aweze kudhaminiwa usalama wake kabla ya kurejea Juba.