Mamia ya wahajiri wa Kiafrika waokolewa katika maji ya pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53687-mamia_ya_wahajiri_wa_kiafrika_waokolewa_katika_maji_ya_pwani_ya_libya
Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza habari ya kuokoa mamia ya wahajiri wa Kiafrika katika operesheni mbili za leo Ijumaa nje kidogo ya mji mkuu Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2019 07:15 UTC
  • Mamia ya wahajiri wa Kiafrika waokolewa katika maji ya pwani ya Libya

Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza habari ya kuokoa mamia ya wahajiri wa Kiafrika katika operesheni mbili za leo Ijumaa nje kidogo ya mji mkuu Tripoli.

Msemaji wa kikosi cha baharini cha Libya, Ayoub Qassem amesema wahajiri 203 wameokolewa wakiwa katika boti mbili za plastiki katika pwani ya Zlitin, umbali wa kilomita 160 mashariki mwa Tripoli.

Ameongeza kuwa, wahamiaji wengine haramu wapatao 87 wameokolewa katika operesheni nyingine iliyofanywa na Gadi ya Pwani ya Libya katika pwani ya Qarabuli, yapata kilomita 50 mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo. 

Msemaji wa jeshi la baharini la Libya amebainisha kuwa, wahamiaji hao wakiwamo wanawake saba na mtoto mdogo mmoja wamekabidhiwa kwa Idara ya Kupambana na Uhamiaji Haramu katika miji ya Khomas na Janzur ambako walianzia safari yao.

Mapema mwezi huu, jeshi la majini la Morocco liliwaokoa wahamiaji haramu 151 kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika wakiwa katika bahari ya Mediterania walipokuwa wakijaribu kuingia barani Ulaya.

Operesheni ya kuwaokoa wahajiri wa Kiafrika

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri waharamu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.

Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakoelekea, bali huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu, kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.