Kuapishwa rais wa Afrika Kusini na mustakbali wa nchi hiyo
Baada ya kupita karibu siku 20 tokea kufanyika uchaguzi mkuu wa bunge nchini Afrika Kusini ambapo chama tawala cha African National Congress ANC kiliibuka mshindi, bunge hilo hatimaye limeidhinisha na kumuapisha Cyril Ramaphosa, rais wa sasa wa nchi hiyo kuhudumia kipindi kingine cha miaka mitano.
Rais Ramapoza amekula kiapo cha kuhudumia nafasi ya rais wa Afrika kusini kwa kipindi kingine cha miaka mitano katika hali ambayo chama tawala cha ANC kinakaniliwa na changamoto nyingi ambazo zimepelekea chama hicho kupoteza umashuhuri wake nchini. Kwa kadiri kwamba katika uchaguzi wa hivi karibuni kilifanikiwa kupata chini ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa. Hicho ni kiwango cha chini zaidi cha kura kuwahi kupewa chama hicho tokea kiingie madarakani baada ya kumalizika mfumo wa ubaguzi wa ragi wa apartheid nchini humo mwaka 1994. Jambo hilo limezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanachama na kupanua pengo la hitilafu ndani ya chama hicho. Suala la ufisadi ambalo limewakumba wanachama wengi wa chama hicho limepelekea chama hicho tawala kupoteza umashuhuri wake mbele ya Waafrika Kusini.
Akizungumzia jambo hilo, Yvonne Daki, Katibu Mkuu wa ANC anayeshughulikia masuala ya majimbo amesema: Rais wa nchi anafanya juhudi kubwa za kupambana na ufisadi na atakabiliana vikali na wale wote wanaopora mali ya taifa. Chama cha ANC kwa sasa kinafanya mabadiliko makubwa ya ndani na bila shaka hatua hii italeta matumaini nchini.
Utendaji dhaifu wa AC umewakatisha tamaa wananchi na hivyo kuwa sababu ya vyama vingine vya upinzani kuibuka na kupata uungaji mkono mkubwa nchini. Vyama hivyo sasa vinafanya juhudi kubwa za kuwavutia vijana ambao ndio wanaopitia machungu ya uhaba wa ajira na hivyo kuweza kuwa na hisa katika madaraka ya nchi pamoja na kuathiri utendaji wa chama tawala. Kama ilivyoshuhudiwa wazi katika uchaguzi wa karibuni, vyama vya upinzani na hata vyenye nisimamo ya kupindukia mipaka viliweza kufanya vizuri katika uchaguzi huo wa bunge ambapo chama kama cha Julius Malema cha Economic Freedom Fighters, kiliweza kujipatia viti 44 katika bunge hilo. Chama hicho kinapigania kutaifishwa sekta kama za madini, benki na kilimo ambazo kimsingi zinamilikiwa na weupe.
Ni kwa muda sasa ambapo Afrika Kusini inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi. Kwa mujibu wa takwimu rasmi nchi hiyo inakabiliwa na kiwago cha chini cha ustawi wa uchumi cha asilimia 1.3, mdororo wa uchumi na uhaba wa ajira wa asilimia 27, ambapo inasemekana karibu watu milioni 9.5 hawana nafasi za kazi. Kukatika umeme mara kwa mara kumezidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo. Shirika la umeme la Eskom ambalo linadhamini asilimia 95 ya umeme wa Afrika Kusini kwa sasa linakabiliwa na deni la dola bilioni 35, jambo ambalo linalifanya lisiweze kuzalisha umeme kwa kiwango kinachohitajika.
Kwa msigi huo, wataalamu wa uchumi wanasema kwamba deni hilo linalolikabili shirika hilo ndiyo changamoto kubwa zaidi kwa uchumi wa Afrika Kusini kwa sasa. Pamoja na hayo, lakini viongozi wa nchi hiyo wameahidi kulitatua tatizo hilo.
Kuhusu hilo, Tito Mboweni Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini amesema: Tuna matumaini makubwa ya kuimarika uchumi baada ya mdororo ulioshuhudiwa mwaka uliopita wa 2018. Tunataraji kuwa pato jumla la ndani litaongezeka mwaka huu wa 2019 na kufikia asilimia 1.5 na mwaka 2021 asilimia 2.
Kulipa madeni, kufanyika marekebisho ya uchumi, kugawa mashamba na kufidia gharama zake pamoja na marekebisho katika sekta ya madini na huduma ya afya ni masuala muhimu katika uchumi wa sasa wa Afrika Kusini. Hata kama Rais Cyril Ramaphosa ametoa ahadi ya kuimarisha uchumi, lakini inaonekana kuwa juhudi zake za kujaribu kukishawishi chama tawala kiunge mkono mipango yake ya marekebisho ya uchumi na vilevile vyama vya upinzani zitakabiliwa na changamoto kubwa.