Wahajiri 2 waaga dunia, 25 watoweka katika ajali ya boti Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53886-wahajiri_2_waaga_dunia_25_watoweka_katika_ajali_ya_boti_libya
Umoja wa Mataifa umesema kuwa wahajiri wawili wa Kiafrika wamekufa maji huku wengine 25 wakitoweka baada ya boti yao kuzama katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterrania, wakiwa katika safari hatarishi ya kuelekea Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2019 01:51 UTC
  • Wahajiri 2 waaga dunia, 25 watoweka katika ajali ya boti Libya

Umoja wa Mataifa umesema kuwa wahajiri wawili wa Kiafrika wamekufa maji huku wengine 25 wakitoweka baada ya boti yao kuzama katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterrania, wakiwa katika safari hatarishi ya kuelekea Ulaya.

Hayo yameripotiwa na Shirika la Kimataifa la Uhajiri la Umoja wa Mataifa IOM. 

Ayoub Gassim, Gadi ya Pwani ya Libya pia amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, operesheni ya kuwaokoa makumi ya wahajiri hao inaendelea.

Amesema miili ya wahajiri hao wawili, ukiwemo wa mwanamke na mtoto mdogo iliopolewa kutoka majini jana Jumapili magharibi mwa mji wa Garaboli, umbali wa kilomita 60 mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Afisa huyo wa Gadi ya Pwani ya Libya amefafanua kuwa, wahajiri 73 wakiwemo watoto wadogo wanane na wanawake 25 wameokolewa na wamepelekwa katika kambi moja ya wakimbizi mjini Tripoli.

Wahajiri wa Kiafrika katika safari hatarishi za kuelekea Ulaya

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya kikosi cha baharini cha Libya kuwaokoa wahajiri 203 wakiwa katika boti mbili za plastiki katika pwani ya Zlitin, umbali wa kilomita 160 mashariki mwa Tripoli.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu hasa kutoka nchi za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.