Mvua na mafuriko yaua watu 9 Puntland, Somalia
Kwa akali watu tisa wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.
Mohammed Abdirahman Dhabancad, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Puntland amethibitisha vifo hivyo na kusema kuwa, miongoni mwa watu walioaga dunia katika majanga hayo ya kimaumbile ni watu watatu wa familia moja.
Amesema eneo lililoathiriwa zaidi na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua zinazonyesha katika eneo la Puntland tokea Ijumaa iliyopita ni mkoa wa Nugaal.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Puntland amebainisha kuwa, mafuriko hayo yametatiza mawasiliano na shughuli za usafiri huku yakipasua barabara kuu inayounganisha Garowe ambayo ni makao makuu ya mkoa huo na mji wa bandari wa Bosaso.

Amesema magari na nyumba zimesombwa na mafuriko hayo katika kijiji cha Sinujiif katika mkoa huo wa Nugaal. Ahmed Elmi Osman, Makamu wa Rais wa Puntland amezuru maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mvua na mafuriko hayo, ambapo ameagiza kubuniwa kamati ya kufuatilia athari za majanga hayo ya kimaumbile.
Hii ni katika hali ambayo, Puntland hivi karibuni ilitangaza kuwa asilimia 70 ya watu wa eneo hilo wanasumbuliwa na ukame kutokana na kutoshuhudiwa mvua kwa muda mrefu.