UN: Raia 42 wameuawa katika mapigano nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54139-un_raia_42_wameuawa_katika_mapigano_nchini_libya
Umoja wa Mataifa umesema mapigano baina ya vikosi vya kamanda muasi wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa katika mji mkuu Tripoli yamesababisha vifo vya raia 42, huku wengine zaidi ya 120 wakijeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2019 08:01 UTC
  • UN: Raia 42 wameuawa katika mapigano nchini Libya

Umoja wa Mataifa umesema mapigano baina ya vikosi vya kamanda muasi wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa katika mji mkuu Tripoli yamesababisha vifo vya raia 42, huku wengine zaidi ya 120 wakijeruhiwa.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, idadi hiyo ni kiwango cha chini mno ambacho kimeweza kuthibitishwa na umoja huo, na kwamba yumkini waliouawa ni wengi zaidi ya idadi iliyotajwa.

Stephane Dujarric, msemaji wa Antonio Guterres amebainisha kuwa, idadi ya watu waliokimbia makazi yao mjini Tripoli kutokana na mapigano hayo, imeongezeka na kupindukia 94 elfu.

Haftar alianzisha vita vya kuwania Tripoli baada ya kukutana na Mfalme wa Saudia mjini Riyadh

Tarehe 4 Aprili mwaka huu Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri ya kushambuliwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Jenerali huyo muasi anaungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa.

Kadhalika Rais wa Marekani, Donald Trump alimpigia simu jenerali huyo akitangaza uungaji mkono wake kwa kile alichodai ni kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa visima vya mafuta vya Libya.