Serikali ya Tanzania: Marufuku watuhumiwa wanawake kukaguliwa na askari wa kiume
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54329-serikali_ya_tanzania_marufuku_watuhumiwa_wanawake_kukaguliwa_na_askari_wa_kiume
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola imesema kuwa, mtuhumiwa mwanamke anayefikishwa katika kituo cha polisi hapaswi kukaguliwa na askari wa kiume na badala yake kazi hiyo inatakiwa kufanywa na askari wa kike, mgambo wa kike au mke wa askari aliyepo karibu na eneo la kituo hicho na si vinginevyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2019 08:47 UTC
  • Serikali ya Tanzania: Marufuku watuhumiwa wanawake kukaguliwa na askari wa kiume

Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola imesema kuwa, mtuhumiwa mwanamke anayefikishwa katika kituo cha polisi hapaswi kukaguliwa na askari wa kiume na badala yake kazi hiyo inatakiwa kufanywa na askari wa kike, mgambo wa kike au mke wa askari aliyepo karibu na eneo la kituo hicho na si vinginevyo.

Waziri Lugola ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma na kufafanua kuwa, endapo kuna mtuhumiwa wa kike amekamatwa katika vituo vya polisi, kutafanyika utaratibu wa kumpata mgambo wa kike wa eneo hilo au mwanamke yeyote mtu mzima mwenye busara anayepatikana kwa urahisi. Awali Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Hamad Masuani alikanusha tuhuma zilizoelekezwa kwa jeshi la polisi la nchi hiyo kwamba limekuwa halizingatii maadili ya kijinsia kwa askari wa kiume kuwakagua watuhumiwa wa kike, huku akiahidi kwamba serikali itapeleka askari wa kike maeneo yote ya lazima baada ya mazingira ya utendaji kazi, hasa makazi kuboreshwa.

Kangi Lugola bungeni

Katika kikao hicho cha bunge mjini Dodoma mbunge wa Geita kupitia chama tawala CCM, Joseph Kasheku Musukuma alihoji ni lini askari wa kike watapelekwa katika kituo cha polisi eneo la Nkome kwa kuwa kituoni hapo upekuzi kwa akina mama umekuwa ukifanywa na askari wa kiume? Akijibu swali hilo Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amesema: “Nimeshamuagiza RPC (Kamanda wa Polisi Geita) kupeleka askari wa kike katika kituo hicho. Taratibu zinaruhusu upekuzi kwa wanawake kufanywa na askari wa kike na kama hayupo basi kazi hiyo ifanywe na mgambo wa kike au mke wa askari.” Amesema Lugola.