Rais Magufuli Tanzania: Watanzania na Wakenya wasikubali kulaghaiwa kwa maneno ya kuwatenganisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54576-rais_magufuli_tanzania_watanzania_na_wakenya_wasikubali_kulaghaiwa_kwa_maneno_ya_kuwatenganisha
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, amesema kuwa, raia wa Kenya na Tanzania wasikubali kulaghaiwa na kupotoshwa kwa maneno yasiyofaa yanayolenga kuwatenganisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2019 11:07 UTC
  • Rais Magufuli Tanzania: Watanzania na Wakenya wasikubali kulaghaiwa kwa maneno ya kuwatenganisha

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, amesema kuwa, raia wa Kenya na Tanzania wasikubali kulaghaiwa na kupotoshwa kwa maneno yasiyofaa yanayolenga kuwatenganisha.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati akiwahutubia wananchi katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita mara baada ya kumpokea mgeni wake, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Kwa mujibu wa rais huyo wa Tanzania, wananchi wa Tanzania na Kenya wanapaswa kuendelea kushirikiana na kulinda uhusiano wao wenye historia kubwa. “Ni azma ya Tanzania kuendelea kuenzi na kutunza uhusiano wetu. Tuendelee kushikamana na kuwa kitu kimoja, tusikubali kulaghaiwa.”

Marais wa Kenya na Tanzania wakifurahia jambo

Amesema Magufuli. Katika upande mwingine, Rais John Pombe Magufuli amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa hatua aliyochukua kufuatia kauli za kibaguzi zilizotolewa na mbunge wa eneo la Starehe, Charles Njagua maarufu kwa jina la 'Jaguar' kuwalenga wafanyabiashara wa kigeni wakiwemo Watanzania wanaojishughulisha nchini Kenya. Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema kuwa kitu anachokitamani katika muda wake wa uongozi ni kuona wana Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaendelea kuwa kitu kimoja. “Mimi kama kiongozi wa Kenya nimesema kama kuna kitu ningependa nione mbele ya wakati wangu, ni sisi wana Jumuiya ya Afrika Mashariki tukiwa kitu kimoja.” Amesema Rais Kenyatta akihutubia wananchi. Aidha Rais Kenyatta amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zitapata maendeleo na kukua, iwapo watu wake watafanya kazi badala ya kuendekeza. Kenyatta ambaye yuko nchini kwa ziara binafsi ya siku mbili amesema haipendezi siasa kutawala muda wote kwani inawazuia watu kufanya kazi za maendeleo. “Tupunguze siasa, tujipange kwa maendeleo. Siasa wakati wake ukifika tutapiga siasa lakini haiwezekani kuanzia asubuhi hadi jioni ni siasa tu hiyo haiwezi kukuza nchi zetu.” Amesema.

Mbunge wa eneo la Starehe, Charles Njagua maarufu kwa jina la 'Jaguar'

Siku chache zilizopita, Jaguar aliibua hali ya taharuki baada ya kutamka kuwa, wafanyabiashara wa kigeni nchini Kenya wanapaswa kuondoka ndani ya saa 24, la sivyo watachukuliwa hatua ya kuwapiga na kuwapeleka uwanja wa ndege. Kauli hiyo iliyozua mvutano mkali nchini Tanzania na kuifanya serikali ya Kenya kutangaza kujitenga na msimamo wa Jaguar, sambamba na kumkamata na kumfikisha mahakamani kutokana na kauli hiyo.