Answarullah: Wasudan waondokane na ubeberu wa Saudia na Imarati
Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen amesema kuwa, raia wa Sudan na nchi yao wanatakiwa kuwa huru mbele ya udhibiti wa vibaraka wa Saudia na Imarati.
Abdul Wahab Al -Mahbashi aliyasema hayo Jumanne katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA ambapo ameongeza kuwa, mapinduzi ya Sudan hayatofikia malengo yake madamu bado nchi hiyo inadhibitiwa na askari ambao ni vibaraka wa Saudia. Akibainisha kuendelea kutumwa vibaraka wa Sudan huko Yemen kutokana na kutokuwepo mabadiliko katika mfumo wa kiutawala nchini Sudan, Al-Mahbashi amefafanua kuwa, raia wa nchi hiyo ni lazima waendeleze mapambano yao kwa ajili ya kufikia ushindi na kuwaondoa madarakani vibaraka hao wa Saudia na Imarati. Aidha amewataka Wasudan kufanya juhudi zitakazofanikisha kurejeshwa nyumbani askari wa Sudan kutoka Yemen.
Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan limekuwa likishikilia uongozi wa nchi hiyo tangu tarehe 11 Aprili, baada ya kumuondoa madarakani Omar al-Bashir. Aidha kuna ushahidi unaoonyesha kwamba Saudia na Imarati zimekuwa zikiliunga mkono baraza hilo la kijeshi la Sudan. Hii ni katika hali ambayo Wasudan wanasisitizia kuundwa serikali ya kiraia. Sudan ilianza kushirikiana na Riyadh na Abu Dhabi tangu mwezi Machi 2015 katika vita dhidi ya taifa masikini la Yemen.