Jul 10, 2019 04:20 UTC
  • Wanaharakati mjini London, Uingereza wataka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky

Wanaharakati wa Kiislamu na wa haki za binadamu mjini London Uingereza wamelaani vikali kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na mkewe na kutoa wito wa kuachiliwa huru wawili hao.

Wanaharakati hao jana walikusanyika mbele ya ubalozi wa Nigeria mjini London ambapo walisikika wakipiga nara za kutaka kuachiliwa huru mara moja Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe.

Aidha waandamanaji hao wamesema kuwa, utendaji wa serikali yya Nigeria na waungaji mkono wake kuhusiana na kadhia ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni fedheha na aibu kubwa. 

Wanaharakati hao wa Kiislamu na wa haki za binadamu wamesisitiza juu ya udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka na asasi pamoja na jumuiya za kimataifa ili kufuatia faili la mwanaharakati huyo wa Kiislamu ambaye anashikiliwa korokoroni kwa miaka kadhaa sasa licha ya mahakama kutoa amri ya kuachiliwa huru. 

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni tarehe 13 Disemba 2015 katika Huseiniya ya Harakati ya Kiislamu huko Zaria kufuatia shambulio la jeshi la nchi hiyo katika Huseiniya hiyo lililopelekea mamia ya Waislamu wa kuuawa.

Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016, kama ambavyo ililiwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa fidia ya dola laki moja na 50 elfu familia ya Sheikh Zakzaky. Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vya Nigeria vimekataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama, na hadi hivi sasa mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.

Tags