Jeshi la Ethiopia kulinda usalama katika mkoa wa Kusini ulioathiriwa na machafuko
(last modified Wed, 24 Jul 2019 03:55:27 GMT )
Jul 24, 2019 03:55 UTC
  • Jeshi la Ethiopia kulinda usalama katika mkoa wa Kusini ulioathiriwa na machafuko

Ethiopia imetangaza kuwa vikosi vya ulinzi na askari usalama wa nchi hiyo ndio watasimamia ulinzi na usalama katika mkoa wa kusini ulioathiriwa na machafuko nchini humo. Machafuko hayo yemeendelea kwa siku kadhaa na kusababisha watu 18 kupoteza maisha.

Taarifa iliyotolewa kupitia televisheni ya mkoa huo imesema kuwa, muundo wa kawaida wa usalama umeshindwa kuhakikisha kunakuwepo na utawala wa sheria na kwamba jambo hilo limechangiwa na sababu mbalimbali. Taarifa zinasema kuwa machafuko hayo yamesababishwa na juhudi za kundi la kikabila la Sidama ambalo ni kundi kubwa zaidi katika mkoa huo wa Kusini za kutaka kuanzisha eneo linalojitawa lenyewe. Suala hilo limeibua mvutano kati ya kundi hilo la Sidama na serikali kuu ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

Itakumbukwa kuwa maandamano yaliibuka wiki iliyopita wakati wanaharakati wa Sidama walipotaka kujitangazia eneo lao wenyewe.  Kwa sasa Ethiopia  ina maeneo tisa yanayojitawala yenyewe. Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, serikali kwanza inapasa kuandaa kura ya maoni kwa ajili ya kuruhusu kundi lolote la kikabila linalotaka kuunda eneo jipya lenye mamlaka yake. Kura hiyo ya maoni itaandaliwa baada ya kundi hilo kuwa limewasilisha ombi lake katika muda wa mwaka mmoja.