Benki ya Dunia yaitahadharisha serikali ya Tanzania kutokana na ongezeko la madeni
Benki ya Dunia imeitahadharisha serikali ya Tanzania kuhusiana na ongezeko la deni la taifa inalodaiwa ndani na nje ya nchi.
Tahadhari hiyo imetolewa kupitia ripoti ya 12 iliyozinduliwa na benki hiyo kuhusiana na hali ya uchumi wa Tanzania na ambayo iliangazia macho umuhimu wa rasilimaliwatu katika kukuza utajiri ambapo pamoja na mambo mengine imetoa ushauri wa namna ya kuboresha ukuaji uchumi na maisha ya wananchi. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia, uwiano wa deni la Taifa na pato la taifa (GDP) kwa mwaka 2018 ulipanda na kufikia asilimia 40.1 kutoka asilimia 37 mwaka uliotangulia.
Aidha ripoti hiyo imeongeza kwamba, ongezeko la mikopo ya kibiashara kutoka kwa mabenki linapaswa kutazamwa kwa umakini mkubwa na serikali ya Dar es Salaam. Hii ni katika hali ambayo taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu inaonyesha kwamba, deni la nje la nchi hiyo linalohusisha lile la umma na sekta binafsi lilikuwa kwa kiasi cha Dola bilioni 21.6 sawa na karibu Shilingi za Tanzania trilioni 49, huku lile la ndani likiwa ni sawa na Shilingi trilioni 15.5. Kutokana na ongezeko hilo, ripoti hiyo imesisitiza kwamba, kwa sasa Tanzania inatumia asilimia 43 ya mapato yake ya ndani kulipa deni la Taifa ingawa ulipaji wa deni la ndani umekuwa mdogo. Kufuatia hali hiyo, Benki ya Dunia imeitahadharisha serikali ya nchi hiyo kuhusiana na suala la ukopaji na ongezeko la madeni. Hii ni pamoja na serikali ya nchi hiyo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayotarajiwa kuboresha masisha ya wananchi.