Chama tawala nchini Afrika Kusini chalaani mashambulio dhidi ya polisi mjini Johannesburg
Viongozi wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC wamelaani mashambulio ya wafanyabiashara ndogo ndogo wa kigeni dhidi ya polisi katika mji wa Johannesburg.
Bunge la Afrika Kusini na chama cha ANC kwa pamoja vimetoa taarifa ya kulaani mashambulio ya wafanyabiashara wa kigeni wasio na leseni za biashara dhidi ya polisi huko Johannesburg na kueleza kwamba, kitendo hicho maana yake ni shambulio dhidi ya serikali.
Pule Mabe, msemaji wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amesema kuwa, kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao cha kuwashambulia polisi kwa mawe hakikubaliki hata kidogo.
Tukio hilo lilitokea siku ya Alkhamisi wakati polisi walipokuwa wakikusanya biadhaa za wafanyabiashara ndogo ndogo wanaofanya biashara zao kinyume cha sheria.
Inaelezwa kuwa, wengi wa wafanyabiashara hao ni raia wa kigeni ambao kimsingi hawana vibali halali vya kuishi nchini Afrika Kusini.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Afrika Kusini imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya hujuma na mashambulio dhidi ya raia wa kigeni.
Makundi yanayowashambulia raia wa kigeni nchini Afrika Kusini yanadai kwamba, wimbi la wageni lililokithiri nchini humo limewaletea matatizo mengi, kubwa zaidi likiwa ni kupungua kwa fursa zao za ajira ambazo zimekuwa zikichukuliwa na wageni hao.
Mara kwa mara makundi ya watu wenye marungu, visu na mapanga huvamia nyumba za raia wa kigeni na kuwafukuza, huku wakipora mali zao.