Aug 15, 2019 12:02 UTC
  • Burundi yaanza kutoa chanjo ya Ebola kwa wahudumu wa afya

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa serikali ya Burundi imeanza kutoa chanjo ya virusi vya ugonjwa hatari wa Ebola kwa wahudumu wa afya hususan wale wanaofanyakazi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya WHO imesema Wizara ya Afya ya Burundi ilianza kutoa chanjo ya Ebola jana Jumatano kwa wahudumu wa afya walioko katika mpaka wa Gatumba ikitumia chanjo aina ya rVSV-ZEBOV.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, chanjo hiyo inatumika kwa ajili ya kuwalinda watu wanaokabiliwa zaidi na hatari ya kuambikizwa virusi vya Ebola na kwamba kipaumbele zaidi kinatolewa kwa wahudumu wa afya walioko katika maeneo hatarishi zaidi.

Hadi sasa hakujaripotiwa kesi hata moja ya maambukizi ya virusi vya Ebola katika nchi ya Burundi. Hata hivyo kuna wasiwasi mkubwa wa ugonjwa huo kuyakumba maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imeathiriwa sana na ugonjwa huo. Ripoti zinasema watu wasiopungua 1800 wamekwishaaga dunia mashariki mwa Congo mwaka huu pekee kutokana na ugonjwa wa Ebola.  

Zaidi ya watu 1800 wameaga dunia Congo DR kutokana na Ebola

Nchi jirani na Congo ya Uganda pia imekuwa katika tahadhari kubwa baada ya watu watatu wa familia moja kuaga dunia kutokana na virusi vya Ebola.  

Wiki iliyopita pia Uganda ilianza zoezi kubwa zaidi la majaribio ya chanjo ya virusi vya Ebola iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa nchi kadhaa za magharibi.  

Tags