Mkutano wa SADC waanza Dar es Salaam
Mkutano wa kilele wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza leo mjini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Mkutano huo wa siku 2 umewaleta pamoja marais wa nchi 12 pamoja na mawaziri kutoka nchi 16 wanachama.
Marais wanaohudhuria kikao hicho ni pamoja na mwenyeji Rais John Magufuli wa Tanzania, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Azali Assoumani wa Comoro Dannye Faure wa Ushelisheli, Joan Manue Goncalves wa Angola, Edgar Lungu wa Zambia, Felix Tshisekedi wa DRC, Andry Rajoelina wa Madagascar, Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Felipe Nyusi wa Msumbuji na Hage Geingob wa Namibia.
Mawaziri wakuu wanaoshiriki ni Ambrose Dlamini wa Eswatini na Motsahai Thabae wa Lesotho huku Malawi ikiwakilishwa na makamu wa rais. Botswana na Mauritius zimetuma wawakilisi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amehutubia kikao hicho cha ufunguzi wa mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Ulinzi umeimarisha kote Dar es Salaam wakati wa mkutano huo utakaomalizika kesho na ambao unahesabiwa kuwa mafanikio makubwa katika sera za kigeni za serikali ya Rais Magufuli.