Tshisekedi atangaza baraza jipya la mawaziri Congo DR
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangaza serikali mpya ya nchi hiyo leo Jumatatu, miezi 8 baada ya Felix Tshisekedi kushinda uchaguzi wa rais.
Katika uchaguzi huo ulioakhirishwa mara kadhaa, Felix Tshisekedi aliwashinda wagombea kadhaa akiwemo mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila. Vyama vya upinzani vilidai kuwa, kulifanyika udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi huo baada ya mazungumzo ya siri yaliyofanyika baina ya Kabila na Tshisekedi.
Wapizani wanasema makubaliano baina ya wawili hayo yalisisitiza kwamba, Kabila atang'atuka madarakani baada ya kuhakikishiwa kwamba ataendelea kuwa na satua na ushawishi mkubwa serikalini.
Thuluthi mbili ya baraza la mawaziri lililotangazwa leo la serikali mpya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inadhibitiwa na washika wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila.
Orodha ya baraza la mawaziri ililotolewa leo na Waziri Mkuu wa Congo DR, Ilunga Ilunkamba ina watu wengi wenye uzoefu mdogo serikalini au wasio na uzoefu kabisa.
Mshirika mkubwa wa Joseph kabila, Ngoy Mukena ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi. Mwezi mei mwaka huu pia Tshisekedi alimteuwa mshirika mwingine mkubwa wa Kabila, Illunga Illunkamba kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.