Tanzania kuwatimua wakimbizi wa Burundi, UNHCR yapinga
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa wakimbizi wote kutoka nchi jirani ya Burundi watarudishwa makwao kuanzi Oktoba lakini Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNCHR limepinga hatua hiyo.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola ametangaza kuwa wakimbizi 2,000 watarudishwa Burundi kuanzia Oktoba Mosi. Lugola amesema hivi sasa kuna amani nchini Burundi na kuongeza kuwa, mashirika ya kimataifa yanawahadaa wakimbizi kwa kuwaambia kuwa hakuna amani Burundi.
Siku ya Jumapili, Waziri Lugola akiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Pascal Brandagiya walitembelea kambi ya wakimbizi ambapo waliwatangazia wakimbizi kuwa watarejeshwa nyumbani.
Hatahivyo, UNHCR ilitoa taarifa Jumanne na kusema hali nchini Burundi haiwaruhusu wakimbizi kurejea. Aidha UNCHR imesema wakimbizi wanaorejea wanapaswa kufanya hivyo kwa hiari na si kulazimishwa.
Dana Huges, msemaji wa UNHCR katika eneo la Mashariki wa Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu amesema karibu wakimbizi 75,000 wa Burundi wamerejea nyumbani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ameongeza kuwa pamoja na hayo, mamia ya watu wanakimbia Burundi kila mwezi na hivyo ametoa wito kwa serikali za eneo hilo kuwa na sera ya kuweka mipaka yao wazi kuwapa hifadhi wakimbizi. Amesema UNCHR itahakikisha kuwa hakuna wakimbizi ambao watalazimishwa kurejea makwao.
Mvutano kati ya shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania kuhusu suala la kuwaregesha makwao wakimbizi wa Burundi umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa sasa.