Serikali ya Tanzania: Umasikini umepungua sana nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55944-serikali_ya_tanzania_umasikini_umepungua_sana_nchini
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kuwa umasikini nchini umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 11, 2019 07:58 UTC
  • Serikali ya Tanzania: Umasikini umepungua sana nchini

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kuwa umasikini nchini umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.

Hayo yameelezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji mjini Dodoma, ambapo ameongeza kwamba mwaka 2012 hali ya umasikini nchini Tanzania ilikuwa kwa asilimia 28.2, lakini mwaka 2018 ilikuwa kwa asilimia 26.8. Dk Ashatu Kijaji amezidi kufafanua kwamba katika kipindi hicho umasikini wa chakula ulipungua kutoka asilimia 9.7 na kufikia asilimia 4.4 mwaka, 2018.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji

Kabla ya hapo mbunge wa Bunda kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), Mwita Getere alihoji kuwa ni lini serikali itaondoa umasikini baada ya kuonyesha mafanikio katika maradhi na ujinga. "Si kweli kuwa umasikini haupungui bali umepungua na unaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa, na hii ni taarifa ya kisomi kutoka kwa watu maalumu." Amesema, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Kuhusu kudhibiti kasi ya ongezeko la ukuaji wa idadi ya watu nchini Tanzania, Dk Kijaji amesema kuwa, ongezeko la watu ni fursa kwa nchi ikiwa fursa zitatumiwa ipasavyo.