Serikali ya Tanzania: Hakuna ugonjwa wa Ebola nchini
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa taarifa ikisema kuwa, hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola ndani ya nchini hiyo, na kuongeza kwamba, watu wawili waliotiliwa shaka na baadaye kupimwa imethibitika kuwa hawana maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na naibu wake, Dk Faustine Ndugulile, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi na jopo la wataalam wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambapo pamoja na mambo mengine, amewataka Watanzania kutokuwa na hofu yoyote kuhusiana na maradhi hayo. Ameongeza kwamba taarifa za kuwepo ugonjwa huo hatari nchini zilitokana na watu wawili kudhaniwa kuwa na maambukizi ya Ebola katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam, suala ambalo halina ukweli wowote.
“Hawa walikuwa wakihisiwa lakini wizara imefanya vipimo vya maabara zaidi ya mara moja kama inavyoelekezwa na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), na kujiridhisha kwamba, hawakuwa na maambukizi ya virusi vya ebola hivyo hakuna ugonjwa huo Tanzania.” Amesema Waziri Ummy. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kuwa, serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiandaa iwapo kutatokea waathirika wa ugonjwa huo nchini na kwamba wamejenga vituo kwa ajili ya watu watakaotiliwa shaka au kuwa na ugonjwa huo mkoani Mwanza, Dar es Salaam na Moshi.