Kadhaa wauawa katika makabaliano baina ya askari wa Misri na magaidi, Sinai
(last modified Sun, 15 Sep 2019 07:16:57 GMT )
Sep 15, 2019 07:16 UTC
  • Kadhaa wauawa katika makabaliano baina ya askari wa Misri na magaidi, Sinai

Vyombo vya usalama vya Misri vimetangaza habari ya kuuawa watu kadhaa katika makabiliano baina ya wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo na wanamgambo huko kaskazini mwa mkoa wa Sinai.

Taarifa ya jeshi la Misri imesema magaidi watatu na askari jeshi watatu waliuawa jana Jumamosi katika kituo cha upekuzi cha Mahajr katika mji wa al-Arish kwenye mapigano hayo.

Habari zaidi zinasema kuwa, makabiliano hayo yalianza baada ya magaidi kuvizia na kuanza kuwafyatulia risasi askari waliokuwa wameshika doria katika kituo hicho. Hakuna kundi lolote la kigaidi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya jana.

Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, jeshi la Misri lilitangaza kuwa limeua magaidi 20 katika operesheni ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kwenye mkoa huo wa Sinai Kaskazini.

Wanachama wa Daesh (ISIS) katika Peninsula ya Sinai, Misri

Siku chache nyuma, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilitangaza habari ya kuuawa askari wanane wa serikali katika shambulizi la magaidi kwenye mji wa al Arish katika mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa nchi hiyo. Aidha magaidi watano waliuawa katika mapigano hayo.

Mapigano huwa yanatokea mara kwa mara baina ya magenge ya kigaidi na jeshi la Misri katika mkoa wa Sinai ulioko kaskazini mwa nchi hiyo na katika baadhi ya maeneo mengine ya Misri.

Tags