Wanachama wa al-Shabaab wakamatwa wakipanga mashambulizi Ethiopia
Serikali ya Ethiopia imetangaza habari ya kuwatia mbaroni wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wakila njama za kutekeleza mashambulizi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa ya Idara ya Kiitelijensia na Usalama wa Taifa ya Ethiopia (NISS) iliyorushwa na shirika la habari la serikali FANA imesema kuwa, wanachama wa genge hilo la ukufurishaji lenye makao makuu yake nchini Somalia wamekamatwa wakiwa katika harakati za ujasusi, baadhi yao wakipiga picha mahoteli na majengo muhimu ya serikali yaliyokuwa yamelengwa katika mashambulizi tarajiwa ya kundi hilo.
Taarifa hiyo ya NISS imeongeza kuwa, "Kundi hilo lilikuwa linajiandaa kushambulia mahoteli, mijumuiko ya kidini na maeneo ya umma katika mji mkuu Addis Ababa."
Idara ya Kiintelijensia na Usalama wa Taifa ya Ethiopia imetangaza kuwa imeshirikiana na Idara ya Ujasusi ya Djibouti kuwatia nguvuni wanachama hao wa al-Shabaab akiwemo kamanda wao, Muhammed Abdullahi katika mji wa Addis Ababa na maeneo ya Oromia na Somali.
Itakumbukwa kuwa, Februari mwaka huu, mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini uliua watu kadhaa wakiwemo wanajeshi wa Ethiopia huko kusini mwa Somalia. Kundi la kigaidi la al-Shabaab kwa upande wake lilidai kuwa limeua wanajeshi 16 wa Ethiopia katika shambulizi hilo.
Siku chache kabla ya shambulizi hilo, jeshi la Ethiopia lilitangaza kuwa linajiandaa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya maficho ya al-Shabaab baada ya kundi hilo kushambulia msafara wa magari ya jeshi la Ethiopia karibu na mji wa Burhakaba kusini mwa Somalia, ambapo kundi hilo la ukufurishaji lilitangaza kuwa limewaua wanajeshi zaidi ya 50 wa Ethiopia.