Fatma Karume: Hatuwezi kuishi kwenye nchi iliyo na dhuluma kiasi hiki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56177-fatma_karume_hatuwezi_kuishi_kwenye_nchi_iliyo_na_dhuluma_kiasi_hiki
Fatma Karume, wakili wa Tanzania aliyevuliwa uwakili na mahkama ya nchi hiyo amesema kuwa hatokata tamaa na kwamba anatafakari kuingia kwenye siasa kwa lengo la kupigania mabadiliko muhimu nchini na kuhakikisha Watanzania wanaheshimiwa na kuzingatiwa misingi ya demokrasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2019 10:16 UTC
  • Fatma Karume: Hatuwezi kuishi kwenye nchi iliyo na dhuluma kiasi hiki

Fatma Karume, wakili wa Tanzania aliyevuliwa uwakili na mahkama ya nchi hiyo amesema kuwa hatokata tamaa na kwamba anatafakari kuingia kwenye siasa kwa lengo la kupigania mabadiliko muhimu nchini na kuhakikisha Watanzania wanaheshimiwa na kuzingatiwa misingi ya demokrasia.

Bi Karume ameyasema hayo leo na kusema: “Mpaka sasa hivi natafakari lakini nataka mabadiliko, hilo I will never give up on (sitolikatia tamaa). Hatuwezi kuishi kwenye nchi iliyokuwa na dhuluma kiasi hiki.” Amesema mwanasheria huyo ambaye pia amewahi kuwa mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na mtoto wa rais wa zamani wa Zanzibar, Abeid Aman Karume. Kwa mujibu wa Karume, amekusudia kuendeleza mapambano yake ya kupigania mabadiliko ndani ya Tanzania hasa iwapo atazuiliwa kuendesha harakati hizo kupitia mahakamani.

Fatma Karume, mwanasheria aliyefutiwa uwakili na mahkama ya Tanzania

Inafaa kuashiria kuwa, Ijumaa iliyopita na mbele ya jaji kiongozi wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, Eliezer Feleshi alitoa uamuzi wa kumvua uwakili mwanasheria huyo kwa madai kuwa katika wasilisho lake kwenye kesi ya Ado Shaibu ya kupinga uteuzi wa Rais Magufuli kwa mwanasheria mkuu wa serikali, Profesa Aderladus Kilangi, aliishambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Adha amesisitiza kuwa, zipo njia nyingi za kutafuta mabadiliko mbali na mkondo wa mahakama, na kwamba miongoni mwa njia hizo ni siasa. “Nataka kuona mahakama inakuwa huru, nataka kuona watu wakienda mahakamani waheshimiwe, wapate haki zao, pengine ni mambo mengi ya kuomba, sijui.” Amesema Fatma Karume.