Raia wanane wa Russia wauawa nchini Libya
Wanajeshi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya wamesema kuwa, shambulio la anga lililofanywa na wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar huko kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya, limeua raia wanane wa Russia.
Wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar walianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji wa Tripoli tangu tarehe 4 Aprili 2019 kwa tamaa ya kuuteka mji huo muhimu.
Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri, Saudi Arabia na Ufaransa zinamuunga mkono Khalifa Haftar, kamanda wa vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya.
Licha ya uungaji mkono wa hali na mali wa nchi zote hizo, lakini hadi hivi sasa jenerali muasi Khalifa Haftar ameshindwa kuingia ndani ya mji wa Tripoli.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, karibu watu elfu moja wameshauawa, zaidi ya elfu tano wameshajeruhiwa na zaidi la laki moja wamekuwa wakimbizi tangu Khalifa Haftar alipoanzisha mashambulizi yake dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, tarehe 4 Aprili mwaka huu.