Wakili wa mwandishi Kabendera amuomba Rais wa Tanzania amsamehe mteja wake
Wakili wa Erick Kabendera, mwandishi hodari wa habari nchini Tanzania aliyetiwa nguvuni zaidi ya miezi miwili iliyopita, amemwomba rais wa nchi hiyo John Magufuli atoe msamaha kwa mteja wake, wakati mahakama ikiakhirisha kwa mara ya sita kusikilizwa kesi ya mwandishi huyo.
Kabendera, ambaye amekuwa akiandika makala katika magazeti ya ndani, ya kanda na ya kimataifa yakiwemo ya The Guardian na The Times of London ya nchini Uingereza, alifunguliwa mashtaka mwezi Agosti ya kuongoza uhalifu ulioratibiwa, kukwepa kulipa kodi na kutakatisha pesa.
Mawakili wake wamepinga mashtaka hayo wakisema kesi ya Erick Kabendera inatokana na sababu za kisiasa, mtazamo ambao unaungwa mkono pia na makundi ya kutetea haki.
Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa jopo la mawakili wa mwandishi huyo wa habari Jebra Kambole, amesema, kwa niaba ya Kabendera na familia yake, anamwomba Rais Magufuli amsamehe mteja wake "ikiwa katika kufanya kazi zake kama mwanahabari, atakuwa amefanya kosa popote pale na kwa namna yoyote ile kwa rais au serikali."
Kambole ameongeza kuwa: "Tunaomba msamaha kwa hilo... tunamwomba (rais) alizingatie ombi hili."
Tarehe 22 ya mwezi uliopita wa Septemba, Rais Magufuli alitangaza kuwa, watu wanaoshikiliwa kwa makosa ya kuhujumu uchumi ikiwemo kukwepa kulipa kodi na kutakatisha pesa wataachiwa huru ikiwa wataungama makosa yao na kurejesha fedha walizoiba.
Erick Kabendera anashikiliwa katika jela yenye ulinzi mkali ya Segerea iliyoko kwenye viunga vya mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam.
Wakati kesi ya mwandishi huyo wa habari iliposikilizwa mara ya mwisho, mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa uchunguzi wake bado haujakamilika, huku mawakili wa mshtakiwa huyo wakitaka mchakato wa kesi uendelezwae, ikitiliwa maanani kwamba mteja wao anashikiliwa kwa makosa ambayo hayaruhusu kupatiwa dhamana.
Asasi za kutetea haki zinadai kuwa, uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania unakandamizwa mno tangu Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015. Kwa mujibu wa asasi hizo, serikali ya Magufuli imeyafungia magazeti kadhaa, imewatia nguvuni na kuwafungulia kesi viongozi wa upinzani pamoja na wanaharakati, sambamba na kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa, hasa vya upinzani. Hata hivyo serikali inakanusha tuhuma za kutumia sera za kiimla na kidikteta katika kuendesha nchi.../