Oct 04, 2019 12:02 UTC
  • Umoja wa Afrika wataka ushirikiano katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola

Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kuwepo ushirikiano zaidi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya kuenea ugonjwa hatari wa Ebola.

Umoja wa Afrika kupitia Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa (Africa CDC) umesema kwenye jarida lake kuwa, ushirikiano katika kupambana na ugonjwa wa Ebola na nchi iliyoathiriwa zaidi na ugonjwa huo yaani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na nchi jirani, utasaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa (Africa CDC), ambacho ni kati ya taasisi za kitaalamu za Umoja wa Afrika, kimesema mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba kitaitisha mkutano mjini Goma kati ya mawaziri wa afya wa DRC na nchi tisa zinazoizunguka nchi hiyo kujadili suala hilo.

Wakati huo huo serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa habari za uvumi kuhusu ugonjwa wa Ebola nchini humo si za kweli.

Idadi ya watu walioaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na homa hatari ya Ebola imefikia 2,014 tangu maradhi hayo yalipuke tena katika nchi hiyo Julai mwaka jana.

Hayo yamo katika tangazo la Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  lililotolewa wiki iliyopita ambalo limeeleza pia kuwa, kesi za maambukizi ya ugonjwa huo zimefikia 3,072.

Chanjo ya Ebola

Kwingineko, serikali ya Tanzania imeendelea kukanusha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo. Taarifa ya serikali imetolewa Alhamisi katika kipindi ambacho mataifa kadhaa ya Magharibi yametoa tahadhari kwa raia wake walioko Tanzania na wale wanaotarajia kuingia nchini humo kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola baada ya taarifa za mwanamke mmoja kudaiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

 

Tags