Marais wa Tanzania na Zambia wafungua kituo muhimu cha mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56436-marais_wa_tanzania_na_zambia_wafungua_kituo_muhimu_cha_mpakani
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na mwenzake Edgar Lungu wa Zambia leo Jumamosi wamefungua kituo muhimu cha huduma za pamoja katika mpaka wa nchi hizo mbili kilichoko Tunduma upande wa Tanzania na Nakonde upande Zambia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2019 10:36 UTC
  • Marais wa Tanzania na Zambia wafungua kituo muhimu cha mpakani

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na mwenzake Edgar Lungu wa Zambia leo Jumamosi wamefungua kituo muhimu cha huduma za pamoja katika mpaka wa nchi hizo mbili kilichoko Tunduma upande wa Tanzania na Nakonde upande Zambia.

Baada ya kufungua kituo hicho, kila mmoja wa marais hao wawili ameingia kwenye chumba cha nchi yake ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kutumika kituo hicho.

Kwa upande wake rais wa Tanzania ameipongeza wizara yake ya fedha lakini zaidi Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA akisema kuwa mwaka huu wamevunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato.

Vile vile amesema, serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na Serikali ya Zambia kurudisha reli ya Tazara na kama kuna watu wanakwamisha marais hao wawili wapeane ahadi za kuwachukulia hatua wakwamishaji hao kwa kila nchi.

 

Ikumbukwe kuwa, Zambia inaongoza kwa kupitisha mizigo mingi kwenye bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo mwaka 2018 asilimia 38 ya mizigo yote iliyopitia bandarini hapo ilikuwa ya Zambia. Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Zambia kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 89.2 bilioni 265.6 za Kitanzania.

Vyombo vya habari vya Tanzania vimesema kuwa, kituo cha Tunduma Nakonde cha mpakani mwa nchi hiyo na Zambia ni moja ya vituo vikubwa Afrika. Kina uwezo wa kupitisha zaidi ya magari 600 kwa siku lakini pia kitaongeza ushindani wa biashara kati ya nchi hizi mbili na kupunguza siku za watu kukaa mpakani.