Oct 16, 2019 04:38 UTC
  • Malawi yakanusha kuwepo Ebola eneo linalopakana na Tanzania

Malawi imekanusha ripoti zilizoenea kwamba mtu mmoja amegunduliwa kuwa na Ebola kwenye eneo la Karonga linalopakana na Tanzania.

Hofu hiyo ilitokea Jumapili wakati wafanyakazi wa afya kwenye eneo hilo waligundua mwanamume mwenye umri wa miaka 37 kuwa na dalili za Ebola.

Afisa wa afya katika eneo hilo,  Louis Tukula amesema mtu huyo alikuwa na maambukizi ya bakteria na si Ebola.

Amesema eneo hilo limekuwa katika hali ya tahadhari tokea ugonjwa wa Ebola uripotiwe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yanaripotiwa wakati ambao Serikali ya Tanzania imefutilia mbali uvumi kwamba kuna visa vya ugonjwa wa Ebola nchini humo.

Pamoja na hayo, nchi kadhaa za Magharibi zimeshatoa tahadhari kwa raia wake wanaosafiri kuelekea nchini Tanzania juu ya ''uwezekano'' wa kuwepo Ebola katika nchi hiyo inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Chanjo ya Ebola

Hayo yanajiri wakati ambao, Shirika la Afya Duniani WHO hivi karibuni limetangaza kuwa juhudi za kuvitokomeza kikamilifu virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaendelea kuzaa matunda.

Idadi ya watu walioaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na homa hatari ya Ebola imefikia 2,014 tangu maradhi hayo yalipuke tena katika nchi hiyo Julai mwaka jana.

Tags