Karibu watu 30 waaga dunia kutokana na mvua kubwa zinazonyesha Tanzania
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo imeongezeka na kufikia watu 29 kutoka 11.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe ameliambia Shirika la Utangazaji nchini Tanzania (TBC) kuwa watu 18 wameaga dunia katika mafuriko yaliyotokea katika wilaya za Korogwe, Handeni, Kilindi na Pangani yaliyosababishwa na mvua kubwa katika siku mbili zilizopita mkoani humo.
Ameongeza kuwa, mvua hizi na mafuriko zimeharibu miundombinu na mashamba ya kilimo, na kwamba sekta ya uchukuzi imeathiriwa pakubwa katika mkoa huo.
Jumanne iliyopita, polisi ya Tanzania ilisema watu 11 wakiwemo wanafunzi watano wamefariki dunia kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mkoani Morogoro.
Maeneo mengi nchini Tanzania kwa sasa yanashuhudia mvua kubwa huku Idara ya Hali ya Hewa nchini humo ikitoa tahadhari ya kuendelea kwa mvua hizo.
Serikali ya Tanzania imewaonya na kuwataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde kuhama maeneo hayo hasa wakati huu ambapo nchi inashuhudia mvua kali ili kuepuka maafa zaidi.