Freeman Mbowe: Chadema tunaamini kwamba CCM imeshindwa kabisa kutekeleza ndoto za Watanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57079-freeman_mbowe_chadema_tunaamini_kwamba_ccm_imeshindwa_kabisa_kutekeleza_ndoto_za_watanzania
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa chama tawala CCM kimeshindwa kutekeleza ndoto za Watanzania za kuwajengea maisha bora na ustawi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2019 11:38 UTC
  • Freeman Mbowe: Chadema tunaamini kwamba CCM imeshindwa kabisa kutekeleza ndoto za Watanzania

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa chama tawala CCM kimeshindwa kutekeleza ndoto za Watanzania za kuwajengea maisha bora na ustawi.

Akitolea mifano suala hilo, Mbowe ameelezea matukio mbalimbali yaliyowahi kujiri nchini humo likiwamo tukio la yeye mwenyewe kushambuliwa kwa bomu akiwa mkutanoni eneo la Soweto jijini Arusha na kusababisha vifo vya watoto na wanawake. Mwenyekiti huyo wa Chadema ameyasema hayo wakati akijitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu Thomas Simba pamoja na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Faraja Nchimbi, huku yeye akiongozwa na wakili Peter Kibatala. Kwa mujibu wa Freeman Mbowe, katika tukio hilo la hujuma ya mabomu ya polisi akiwa katika mkutano jijini Arusha, hakuna mtu yeyote aliyewahi kufikishwa mahakamani kama ambavyo hata ombi lao la kutaka uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na watu kutoka nje ya nchi lilikataliwa na serikali.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Amezidi kubainisha kwamba: “Chadema tunaamini CCM imeshindwa kutekeleza ndoto ya Watanzania ya kujenga maisha bora na ustawi wao, kwa sababu kumekuwapo na matukio mbalimbali kwenye nyanja za ulinzi, usalama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.” Ameeleza. Aidha mwanasiasa huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania amedai kuwa wapi viongozi mbalimbali wa Chadema wameuawa kwa matukio ya kutatanisha na kwa nyakati tofauti, wakiwamo wanahabari na wanaharakati. Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo inayowakabili viongozi tisa wa chama hicho, amedai mahakamani kuwa, mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa na polisi eneo la Nyororo mkoani Iringa. Kuhusu tukio la kushambuliwa kwa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbowe alieleza kuwa lilitokea saa 7:00 mchana Septemba 7, 2017 Dodoma na hadi sasa hakuna uchunguzi uliofanyika, hakuna taarifa ya kufikishwa mahakamani kwa mtu yeyote akihusishwa.

Kulia, ni Daud Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa habari na kushoto ni Akwilina Akwilini, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), wanaodaiiwa na wapinzani kuwa waliuawa na jeshi la polisi Tanzania

Mfano mwingine  Mbowe amezungumzia sakata la kutoweka aliyekuwa msaidizi wake, Ben Sanane, ambapo amesema kuwa alitekwa takriban miaka miwili iliyopita na waliiomba serikali kuleta wachunguzi wa kimataifa lakini pia ilikataa. Aidha amezungumzia tukio la kukamatwa Daniel John aliyekuwa katibu kata ya Kinondoni kupitia chama cha Chadema na gari ya walinzi wa CCM akiwa na mwenzake ambapo alipigwa na kuteswa.