EUROMONEY: Ustawi Tanzania utadorora kutokana na ukandamizaji wa kisiasa
Jarida la Euromoney limesema Tanzania itakumbwa na matatizo ya kutekeleza mahitajio yake ya miundo msingi kutokana na hali ya kisiasa yenye kuibua changamoto.
Jarida hilo limewanukulu weledi wa mambo wakisema hali ya kisiasa nchini Tanzania imepelekea wawekezaji wa kimataifa na nchi wafadhili kujiweka mbali na nchi hiyo.
Akizungumza na Euromoney, George Bodo, mkuregenzi katika taasisi ya utafiti ya Callstreet Research and Analytics amesema, uwekezaji umepungua nchini Tanzania kutokana na kile alichokitaja ni sera za Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo. Hata hivyo amesema Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika zinatazamiwa kuendelea kuipa Tanzania misaada ya kifedha.
Mwezi Oktoba mashirika mawili ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yalisema ukandamizaji wa serikali ya Tanzania dhidi ya vyombo vya habari, watetezi wa haki za binadamu na vyama vya upinzani umeongezeka tangu mwaka 2015. Mashirika hayo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu sasa yanaitaka serikali ya Tanzania kuheshimu haki za raia wake.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa kuzindua Kituo kipya cha uwanja wa ndege wa Julius Nyerere mjini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema Tanzania siyo masikini na ipo tayari kujiamulia mambo yake na kwamba tayari inatekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo.