Hali ya kisiasa Tanzania kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa
Huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania, chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndio chama tawala kimetoa taarifa ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu ya jana mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole alisema kuwa hakuna shaka yoyote kwamba chama hicho kitapata ushindi. “Tuliambiwa hapa Arusha Mjini ni ngome ya mbunge fulani wa chama cha bwana Mbowe, Arusha wakati wote imekua ya CCM na sasa namwambia mbunge wa hapa atafute kazi nyingine mwaka 2020, nimesikia eti anaenda kugombea Kilimanjaro huko asijisumbue tumeshamaliza kazi.” Alisema Polepole.
Kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) imetolewa katika hali ambayo hadi sasa jumla ya vyama sita vya upinzani vimetangaza uamuzi wao wa kususia uchaguzi wa serikali za mitaa nchini humo. Vyama hivyo ambavyo ni pamoja na chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT- Wazalendo, UPDP, chama cha Wananchi (CUF), Chauma na NCCR-Mageuzi kwa nyakati tofauti vimetangaza kuwa, vimechukua uamuzi huo kutokana na kutotendewa haki wagombea wao, ikiwa ni pamoja na kunyimwa fursa ya kuchukua fomu za kugombea katika ofisi za watendaji au kushindwa kurejesha fomu hizo kwa sababu mbalimbali.
Katika hatua nyingine chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka Tume ya Uchaguzi kuacha kutumia jina na nembo ya Chadema katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa sababu chama hicho tayari kimejitoa kwenye uchaguzi huo. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Bara, John Mnyika hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari kwamba, chama hicho kimejitoa kwa sababu ya dhuluma zilizofanyika kwenye mchakato mzima wa uchaguzi. Kwa mujibu wa Mnyika, chama hicho kilichukua uamuzi wa kutotumiwa jina na nembo ya Chadema katika uchaguzi huo, kwa kuwa kuna baadhi ya wagombea wanakusudia kushiriki uchaguzi huo kwa kutumia jina na nembo ya chama hicho.
Katika uwanja huo naye Mwenyekiti wa chama cha National League For Democracy (NLD) ambacho pia ni chama cha upinzani Bwana Oscar Emmanuel Makaidi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, chama hicho hakitashiriki uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji mkubwa na wa makusudi wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi. Hata hivyo siku chache baadaye Katibu Mkuu wa chama hicho Tozy Matwanga alijitokeza na kueleza kuwa Kamati Kuu ya NLD haitambui uamuzi huo. Kwa mujibu wa Matwanga, Makaidi alifanya maamuzi binafsi na ya haraka bila kushirikiana na Kamati Kuu jambo ambalo ni uvunjaji wa katiba ya chama.
Miito ya kuakhirishwa uchaguzi huo nayo imetolewa na pande mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini nchini Tanzania. Katika uwanja huo askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa Owdenburg Mdegela, hivi karibuni alinukuliwa akitoa mwito wa kuahirishwa uchaguzi huo na kusema kuwa ni vizuri kwa wanasiasa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwanza ili kupata suluhisho linaloweza kusaidia vyama hivyo kuingia kwenye chaguzi.
Mdegela alisisitiza kuwa, hakufurahishwa kabisa na hatua ya wapinzani kujitoa katika uchaguzi, kwani upinzani unahitajika ili kuweka mambo sawa.
Huku hali ikiwa hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi imesema kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika kama ulivyopangwa tarehe 24 mwezi Novemba mwaka huu.
Katika mazingira hayo hivi sasa Tanzania inatawaliwa na anga mbili za kimtazamo. Upande wa kwanza ni ule unaounga mkono uamuzi wa vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo, na kwamba suala hilo sambamba na kuipaka matope serikali ya Dar es Salaam chini ya Rais John Pombe Magufuli kimataifa, pia litaishinikiza serikali hiyo itayarishe mazingira bora ya kidemokrasia kwa ajili ya upinzani. Na upande wa pili ni ule unaoamini kwamba, vyama hivyo vinatakiwa kushiriki uchaguzi huo na kwamba kujiondoa hakuwezi kuishinikiza serikali kutekeleza matakwa yao. Upande wa pili unatumia hoja kwamba, hata wakati wapinzani visiwani Zanzibar waliposusia uchaguzi wa marudio mwaka 2015, serikali ya CCM iliendesha zoezi la uchaguzi huo bila ya ushiriki wa upinzani hapo tarehe 20 Machi 2016 na kumtangaza Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi wa urais kwenye uchaguzi huo. Licha ya ususiaji huo wa upinzani hadi Dk. Shein ameendelea kuwa rais huku upinzani nao ukishindwa kufikia malengo yake.
Alaakullihal, uamuzi sahihi na kama walivyoshauri weledi wengi wa mambo nchini Tanzania ni kufanyika mazungumzo chanya kati ya serikali na vyama vya upinzani kwa ajili ya kutatuliwa hitilafu na tofauti zinazohusiana na suala zima la uchaguzi nchini humo.