Mahakama imeakhirisha kwa mara ya nane kusikiliza kesi inayomkabili mwandishi habari Kabendera
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57389-mahakama_imeakhirisha_kwa_mara_ya_nane_kusikiliza_kesi_inayomkabili_mwandishi_habari_kabendera
Mahakama nchini Tanzania leo imeakhirisha kwa mara ya nane kusikiliza kesi inayomkabili mwandishi habari mashuhuri wa nchi hiyo aliyekamatwa mwezi Julai mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2019 09:49 UTC
  • Mahakama  imeakhirisha kwa mara ya nane kusikiliza kesi inayomkabili mwandishi habari Kabendera

Mahakama nchini Tanzania leo imeakhirisha kwa mara ya nane kusikiliza kesi inayomkabili mwandishi habari mashuhuri wa nchi hiyo aliyekamatwa mwezi Julai mwaka huu.

Mawakili wanaomtetea mwandishi huyo wa habari na makundi ya kutetea haki za binadamu wamesema kuwa kesi dhidi ya Eric Kabendera imetokana na masuala ya kisiasa.

Polisi ilimtia mbaroni mwandishi habari Eric Kabendera mwenye makao yake jijini Dar es Salaam ambapo alishtakiwa mwezi Agosti mwaka huu kwa makosa ya kuongoza jinai zilizoratibiwa, kushindwa kulipa kodi na kutakatisha pesa. Hata hivyo mawakili wanaomtetea mwandishi huyo wa habari wamepinga tuhuma hizo dhidi ya mteja wao. Hadi kufikia sasa hakuna kesi iliyosikilizwa dhidi ya Kabendera. Katika vikao vyote nane vilivyotazamiwa kusikilizwa tangu mwezi Agosti mwaka huu; waendesha mashtaka wameiambia mahakama kuwa uchunguzi bado haujakamilika.

Mwezi uliopita, wakili anayemtetea Erick Kabendera, Jebra Kambole aliiambia mahakama kuwa anafanya jitihada ili mteja wake apatiwa ahueni katika kesi inayomkabili.

Wakili Jebra Kambole akiwa na mteja wake mwandishi habari, Eric Kabendera

Wakati huo huo makundi ya kutetea haki za binadamu yameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania umebanwa tangu Rais John Magufuli aingie madarakani mwaka 2015. Serikali tayari imefunga baadhi ya magazeti na tovuti kadhaa pamoja na kuwatia nguvuni viongozi wa upinzani na kuzuia mikutano ya kisiasa. Serikali kwa upande wake imekanusha ukosoaji huo dhidi yake kwamba inabana uhuru wa vyombo vya habari.