Tundu Lissu: Ninaogopa kurudi Tanzania halafu nipigwe tena risasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57577-tundu_lissu_ninaogopa_kurudi_tanzania_halafu_nipigwe_tena_risasi
Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kwamba, atarejea nchini humo baada ya  marafiki zake kumhakikishia usalama wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2019 08:59 UTC
  • Tundu Lissu: Ninaogopa kurudi Tanzania halafu nipigwe tena risasi

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kwamba, atarejea nchini humo baada ya  marafiki zake kumhakikishia usalama wake.

Lissu ameyasema hayo  katika mahojiano na kituo cha televisheni cha KTN cha nchini Kenya baada ya kuulizwa swali na mtangazaji Paul Nabiso kuhusu mpango wake wa kurejea nchini baada ya kumaliza matibabu yake nje ya nchi. Kadhalika mwanasiasa huyo wa Chadema amesema: “Hali ya usalama wangu bado si nzuri, nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani kesho na keshokutwa ninapigwa risasi tena. Bado kuna vitisho vya aina hii,  watu wenye busara lazima wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama.” Amesema Tundu Lissu. Akizungumzia iwapo jitihada hizo tayari zinaendelea kutekelezwa amesema: “Hizi jitihada zinafanywa na marafiki wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha nakuwa salama kurudi Tanzania. Ikifika mahala wakasema usalama wangu utaangaliwa nitarudi nyumbani.”

Gari la Lissu siku aliposhambuliwa na watu wasiojulikana

Hayo yanajiri ambapo tarehe 9 Oktoba mwaka huu mwanasheria mkuu huyo wa Chadema alisema kuwa hawezi kurejea Tanzania kwa kuwa mazingira ya  usalama wake si mazuri. Kabla ya hapo yaani tarehe 7 Septemba mwaka huu  Lissu alikaririwa akisema kwamba, atarejea Tanzania mchana kweupe akitokea Ubelgiji alikoenda kutibiwa, na kwamba suala hilo halitakuwa siri kama ambavyo anashauriwa na watu wengi. Hata hivyo katika mahojiano ya jana, Lissu amesema: “Tunazungumzia mtu ambaye amepigwa risasi 16, amefanyiwa operesheni 24 katika kipindi cha miaka miwili. Ni makosa kiasi gani kuuliza mtu aliyefanyiwa hivi na watu ambao hawajakamatwa mpaka leo akirudi atakuwa salama au la, ni makosa kiasi gani kuuliza swali kama hilo.” Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge hapo tarehe 7 Septemba 2017.