UN yatuma wanajeshi katika eneo lililokumbwa na mapigano ya kikabila Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umetuma kikosi cha askari wake wa kulinda amani katika eneo la katikati mwa Sudan Kusini ambako watu karibu 80 wameuawa katika mapigano ya kikabila.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema askari wa kulinda amani wa umoja huo kutoka Nepal wametumwa katika eneo hilo baada ya maafisa wa serikali kuripoti kuwa makumi ya raia wameuawa katika mapigano ya kikabila.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini katika jimbo la Western Lakes, Benjamin Laat amesema mapigano baina ya makabila ya Gek na Manuer yaliibuka tarehe 27 Novemba baada ya raia mmoja wa jamii ya Manuer kuuawa na vijana wa kabila la Guk.
Nchi ya Sudan Kusini iliyojetenga na Sudan na kujitawala mwaka 2011 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili baadaye baada ya Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kwamba alifanya jaribio la kumuondoa madarakani.
Vita hivyo ambavyo vimesababisha mauaji ya watu wasiopungua laki nne vimezusha njaa na mgogoro mkubwa wa wakimbizi ambao haujawahi kushuhudiwa barani Afrika baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.