Watu wasiopungua 265 wapoteza maisha katika mafuriko Afrika Mashariki
(last modified Sat, 07 Dec 2019 04:04:31 GMT )
Dec 07, 2019 04:04 UTC
  • Watu wasiopungua 265 wapoteza maisha katika mafuriko Afrika Mashariki

Mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko katika nchi za Afrika Mashariki katika kipindi cha miezi miwili iliyopita zimeuwa watu wasiopungua 265.

Televisheni ya France 24 imeripoti kuwa watu wasiopungua 265 wameaga dunia na maelfu ya wengine wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko huko Kenya, Burundi, Tanzania, Sudan Kusini, Uganda na Ethiopia. Mvua hizo zimeziathiri nchi hizo za eneo la mashariki mwa Afrika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. 

Mafuriko Afrika Mashariki
 

Huko Kenya watu 132 wameaga dunia huku Burundi wengine 37 wakipoteza maisha kufuatia mafuriko hayo. 

Huko Uganda watu kadhaa wamefukiwa na udongo baada ya mvua kubwa kunyesha. Wakati huo huo serikali ya Sudan Kusini imetangaza hali ya hatari katika eneo la Kobo kufuatia kuathiriwa pakubwa na mafuriko. Mashamba katika eneo hilo yamefunikwa na maji huku makumi ya familia zikikosa makazi. Ongezeko la joto katika nchi za Afrika Mashariki limesababisha kutokea mafuriko hayo tajwa.