Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko Burundi yafika 43, Uganda 22
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57755-idadi_ya_waliokufa_kutokana_na_mafuriko_burundi_yafika_43_uganda_22
Idadi ya watu walipoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki imeongezeka.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 08, 2019 12:10 UTC
  • Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko Burundi yafika 43, Uganda 22

Idadi ya watu walipoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki imeongezeka.

Habari kutoka Bujumbura zinasema kuwa, makumi ya watu wamefariki dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua hizo nchini Burundi.

Duru za habari zinaarifu kuwa, maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo la Jibitoke, wilayani Mubina yamesababisha watu 38 kupoteza maisha.

Aidha watu watano wameaga dunia baada ya kusombwa na maji kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika mji mkuu wa zamani nchi hiyo, Bujumbura.

Nchini Uganda, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko katika wilaya ya magharibi ya Bundibugyo imeongezeka na kufikia 22. 

Athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Afrika Mashariki

Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Mutegeki Ronald amesema leo Jumapili kuwa, watu wengine kadhaa hawajulikani walipo kufuatia mafuriko hayo katika kijiji cha Bumpomboli, kaunti ndogo ya Harugale. Mafuriko hayo yalisababishwa na kuvunjika kingo za Mto Tokwe jana Jumamosi.

Huko Kenya watu 132 wameaga dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua hizo ambazo zinashuhudiwa katika kanda ya Afrika Mashariki kwa miezi miwili sasa.