Dec 15, 2019 13:27 UTC
  • Omar al Bashir
    Omar al Bashir

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wananchi wa Sudan hawakuridhishwa na hukumu ya kifungo cha miaka miwili katika kituo cha marekebisho ya kitabia iliyotolewa dhidi ya kiongozi aliyeondolewa madarakani wa nchi hiyo, Omar al Bashir, baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma na ufisadi.

Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa, wahanga wa ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na utawala wa miaka 30 wa al Bashir wanataka kutendewa haki na uadilifu kutokana na jinai za kutisha zilizofanywa na jeshi la rais huyo wa zamani.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kanda ya Afrika, Jehanne Henry amesema kuwa, hatia zinazohusiana na ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi zinatofautiana na jinai na ukiukaji wa haki za binadamu waliofanyiwa Wasudan wengi wakati wa utawala wa Omar al Bashir. Jehanne Henry ameongeza kuwa, kwa sababu hiyo Wasudani wengi hawaridhishwi na hukumu ya kifungo cha miaka miwili katika kituo cha marekebisho ya tabia iliyotolewa jana Jumamosi na mahakama ya Khartoum.

Gazeti la New York Post limeripoti kuwa, kesi ya Omar al Bashir inatazamwa kama mtihani mkubwa kuhusu uwezo na nia ya serikali mpya ya Khartoum ya kutenda haki kwa wahanga wa ukatili na jinai zilizofanywa na mtawala wa zamani wa nchi hiyo na kuhusu mabadiliko halisi ya kisiasa nchini humo baada ya kuondolewa madarakani kwa mashinikizo ya wananchi.

Gazeti hilo limenadika kuwa: "Dikteta huyo wa zamani wa Sudan mwenye umri wa miaka 75 anasakwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita na mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan."

Jaji wa mahakama ya Khartoum al Sadiq Abdelrahman alisema jana kwamba: "Mahakama imempata Omar Hassan al Bashir na hatia na imeamua kumpeleka katika kituo cha kijamii cha kurekebisha tabia kwa muda wa miaka miwili." 

Al Bashir amepatikana na hatia ya kupora mali ya umma

Baada ya kutolewa hukumu hiyo baadhi ya Wasudani walionesha mshangao wao mkubwa katika mitandao ya kijamii wakisisitiza udharura wa kufanyika marekebisho ya kimsingi katika idara za mahakama na vyombo vya sheria vya nchi hiyo ambavyo wamesema bado vinadhibitiwa na wafuasi wa al Bashir.

Tags